Kila sekunde tano hewa chafu inachukua uhai wa mtu duniani

Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016

Spread the love

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa amesihi serikali duniani zichukue hatua kuondokana na uchafuzi wa hali ya hewa kama wajibu wao wa kutekeleza haki za binadamu.

Mtaalamu huyo David Boyd ambaye anahusika na haki za binadamu na mazingira amesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

“Uchafuzi wa hewa ni muuaji wa taratibu, asiyeonekana na anahusika na vifo vya mapema vya watu milioni 7 kila mwaka, wengi wao wakiwa ni wanawake, na watoto na jamii maskini,” amesema Bwana Boyd akiongeza kuwa takwimu hizo ni sawa na mtu kufariki dunia kila baada ya sekunde tano.

Amesema kwamba kushindwa kuhakikisha uwepo wa hewa safi ni kinyume na haki ya binadamu ya uhai, afya na ustawi pamoja na haki ya kuishi katika mazingira yenye afya.

Kwa mantiki hiyo amesema, “serikali lazima zichukue hatua za dharura kuboresha kiwango cha hali ya hewa na kwa kufanya hivyo zitakuwa zinatimiza wajibu wao wa haki za binadamu.”

Amesisitiza kuwa haki ya mazingira yenye afya ni msingi wa ustawi wa binadamu na inatambuliwa na zaidi ya mataifa 150 katika ngazi ya taifa na kikanda hivyo amesema, “haki hii inapaswa kupatiwa msisitizo kimataifa ili kuhakikisha haki hii inafurahiwa na kila mtu, popote alipo huku misingi ya haki za binadamu duniani na kutokubaguliwa ikizingatiwa.”

Chanzo: UN

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *