Rasilimali na teknolojia ndio changamoto ya kutekeleza SDGs Tanzania:Waziri Mpango

Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha wa Tanzania wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya UN kando mwa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu utekelezaji wa SDGs. (18 July 2019). Picha na UN News

Spread the love

Tukifanikiwa katika rasilimali na teknolojia Tanzania tutapiga hatua kubwa sana katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, ifikapo mwaka 2030,

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa fedha na mipango wa nchini hiyo Dkt. Philip Mpango alipozungumza na UN News idhaa ya kiswahili kandoni mwa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa HLPF linalotathimini utekelezaji wa malengo hayo kwa nchi wanachama 50 waliojitolea kufanyiwa tathimini ikiwemo Tanzania.

Waziri mpango amesema wamepiga hatua kubwa katika baadhi ya malengo ikiwemo , usawa wa kijinsia, elimu na hata ukuzaji wa uchumi hasa kwa kuanzisha viwanda vingi ambavyo mbali ya kukuza uchumi vinatoa ajira kwa maelfu ya watu wakiwemo vijana ambao ndio idadi kubwa ya watu wa taifa hilo, hata hivyo amesema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto kubwa.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni, “ya kwanza kubwa ni rasilimali, rasilimali fedha na rasilimali watu za kutekeleza malengo haya. Malengo ni mengi . Lakini rasilimali fedha kwa kiwango cha nchi yetu ambapo tumefika hivi sasa ni changamoto, kwa hivyo tunafanya juhudi kubwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani lakini hayatoshi. Ni kwamba tuna fedha nyingi pia zinatoroshwa nchini, kwa maana ya madini yetu, na juzi juzi tu tuliwaonesha watanzania jinsi ambavyo dhahabu yao ilikuwa inatoroshwa tu, wengine walikuwa wameweka kwenye mahindi. Wengine wanakata matikiti maji wanaweka humo dhahabu na zinatoroshwa nje.  Lakini wapo we ngine ni wajanja zaidi ambao wanapeleka fedha zenyewe, wanazipeleka huko nje zinakaa kwenye akaunti za huko nje, kwa hiyo hili ni eneo moja ambalo tunahitaji pia msaada wa kimataifa ili kuweza kudhibiti zibakie nchini.” 

Waziri mpango ameongeza kuwa mtihani mwingine ni teknolojia.

“Amesema zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wetu vijijini wanatumia kuni kwa ajili ya mahitaij ya nishati ya kupika. Gesi ipo lakini nchi yetu si  ndogo na watanzania si wachache kwa hiyo mpaka uweze kufikisha hiyo huduma ya gesi vijijini bado unahitaji kuwekeza. Mfano zipo teknolojia za kutengeneza mkaa kutokana na mabaki ya pumba ya mpunga na kadhalika na hazijasambaa kwenye nchi yetu. Zipo teknolojia mfano kutoka Iceland wao wana teknolojia ya viwandani ambayo inanyonya hewa ya ukaa na kugeuza kuwa mawe. Kumbe teknolojia kama hizi zingetusaidia. Zipo teknolojia za kutumia ndege zisizo na rubani kupeleka damu vijijini kusaidia wanawake wanaofariki dunia wakati wa kujifungua wanapoteza damu nyingi, na  sisi tumeanza kidogo kule Mwanza lakini hizi ni teknolojia ambazo zingeweza kutusaidia kupunguza vifo vya wajawazito na hata kupeleka elimu vijijini.”

Dkt. Mpango alikuwepo jijini New York, Marekani kuhudhuria jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu  utekelezaji  wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambapo Tanzania kwa mwaka huu ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyojitolea kuwasilisha kwa hiari utekelezaji wa malengo hayo yaliyopitishwa mwaka 2015 na ukomo wake ni mwaka 2030.

Chanzo:UN Kiswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *